Nenda kwa yaliyomo

Malaki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nabii Malaki alivyochorwa na Duccio di Buoninsegna, 1310-1311 hivi, Siena, Italia).

Malaki (kwa Kiebrania מלאכי) alikuwa nabii aliyetoa ujumbe unaopatikana katika kitabu cha mwisho kati ya vitabu 12 vya Manabii wadogo ambavyo, pamoja na vingine vingi, vinaunda Tanakh, yaani Biblia ya Kiebrania. Hivyo ni pia sehemu ya Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo, na kwa kuwa humo vitabu vya manabii vinapangwa baada ya vitabu vya hekima, kitabu cha Malaki ni cha mwisho kabla ya vitabu vya Agano Jipya.

Jina lake halisi halijulikani, hivyo linatumika lile la neno muhimu zaidi la kitabu, "Malaki", lenye maana ya "Mjumbe wangu".

Yaliyomo yanawezesha kukisia kiliandikwa lini, yaani baada ya Hekalu la Yerusalemu kuwekwa wakfu (515 KK), na kabla ya katazo la ndoa za mseto kati ya Wayahudi na mataifa mengine lililotolewa na Nehemia (445 KK); sanasana ni karibu na mwaka huo.

Ndipo alipotabiri ujio wa siku ya Bwana na kuingia kwake hekaluni, pamoja na kwamba daima na popote sadaka safi inatakiwa kutolewa kwa heshima ya jina lake [1].

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 18 Desemba[2] lakini pia 3 Januari au 14 Januari[3].

Muhtasari wa kitabu

[hariri | hariri chanzo]

Kitabu kinaundwa na sehemu sita za namna ileile: Mungu (au nabii wake) anatoa kauli ambayo inajadiliwa na waamini na makuhani wao, halafu inafafanuliwa katika hotuba inayochanganya vitisho na ahadi za wokovu.

Mada kuu ni mbili: makosa ya makuhani na waamini wengine katika ibada, halafu makwazo yanayosababishwa na ndoa za mseto.

Nabii anatabiri siku ya YHWH atakayetakasa makuhani, ataangamiza waovu na kuwapa ushindi waadilifu.

Mistari ya mwisho, ikitabiri ujio wa pili wa nabii Eliya, ilivutia sana tumaini la Wayahudi; ndiyo sababu ilijadiliwa sana kuhusiana na Yohane Mbatizaji na Yesu Kristo, kama inavyoonekana katika sehemu mbalimbali za Injili.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Malaki kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.