Hizbullah ya Lebanon
- Makala hii inahusiana na Hizbullah ya Lebanon. Ili kufahamu mafuhumu yenye anuani kama hii hii angalia makala ya Hizbullah.
Hizbullah (Kiarabu: حزب الله (لبنان)) ni kundi la kisiasa na kijeshi la Kishia la nchini Lebanon. Harakati ya Hizbullah ya Lebanon iliasisiwa mwaka 1982 kwa shabaha ya kukabiliana na utawala haramu wa Israel. Kundi hilo liliasisiwa kwa himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hizbullah ilianzisha harakati zake dhidi ya Israel kwa operesheni za kujitolea kufa kishahidi. Kisha baadaye ikaongeza nguvu zake za kijeshi na ikawa ikikabiliana na Israel kwa makombora ya Katisha na vita vya msituni.
Katibu Mkuuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ni Sayyid Hassan Nasrullah. Kabla yake Sayyid Abbas Musawi ndiye alikuwa akishikilia wadhifa huo kabla ya kuuawa shahidi. Aidha Katibu Mkuu wa kwanza wa harakati hiyo alikuwa Sheikh Subhi Tufayli. Hadi sasa Hizbullah ya Lebanon imeshapigana vita kadhaa vya kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo miongoni mwa vita hivyo ni vile Vita vya Siku 33. Israel ilianzisha vita hivyo kwa lengo la kuipokonya silaha Hizbullah na kuwakomboa wanajeshi wake wawili waliokuwa wamekamatwa mateka katika operesheni ya Hizbullah iliyojulikana kwa jina la al-Wa'd al-Sadiq (Ahadi ya Kweli).
Hizbullah ilishiriki pia katika vita vya kupambana na wanamgambo wa kitakfiri huko Syria kwa shabaha ya kuiunga mkono serikali ya nchi hiyo. Hizbullah ina harakati pia za kiutamaduni, kiijami na kisiasa. Kanali ya Televisheni ya al-Manar inamilikiwa na Hizbullah.
Historia Fupi na Sababu ya Kuundwa Hizbullah
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon, iliundwa mwaka 1982 kwa himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran. [1] Katika miaka kadhaa ya awali, Hizbullah iliendesha kwa siri harakati zake dhidi ya utawala vamizi wa Israel. Novemba 11, 1984, Ahmad Ja'far Qasir alitekeleza operesheni ya kujitolea kufa shahidi dhidi ya wanajeshi wa Israel kusini mwa Lebanon ambapo askari kadhaa wa utawala huo vamizi waliangamizwa. Februari 16, 1985 sambamba na kuondoka Israel huko Saida, Hizbullah ilitangaza kuhusika na operesheni ya kujitolea kufa shahidi ya Ahmad Ja'far Qasir na kutangaza rasmi itikadi na stratejia yake ya kukabiliana na Israel. [2]
Hussein Dehqan, mmoja wa makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema, baada ya operesheni ya Baytul-Muqaddas mwaka 1361 Hijiria Shamsia katika vita baina ya Iran na Iraq, utawala wa Israel uliishambulia Lebanon. Kundi la makamanda wa jeshi la SEPAH lilitumwa huko Lebanon kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vikosi vya Lebanon kwa minajili ya kukabiliana na Israel. Makamanda hao sambamba na kutoa mafunzo ya kijeshi, walikuwa na jukumu pia la kuleta umoja baina ya makundi yenye uhusiano na Iran ambapo hatimaye juhudi zao zilipelekea kuundwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon. [3] Sheikkh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema: Imam Ruhullah Khomeini alituma kundi la makamnda hao Lebanon kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vikosi vya Lebanon. Hata hivyo makundi na mirengo ya Harakati ya Amal, Hizb al-Daawah, Tajamu’ ulamaa Beqaa na kamati za Kiislamu zilikuwa zimeafikiana kuunda chama kimoja mkabala na uvamizi wa Israel na mpango wa hilo pia ulikuwa umekubaliwa na Imam Khomeini. [4]
Uongozi
Katibu Mkuu wa kwanza wa Hizbullah ya Lebanon alikuwa Subhi Tufayli ambaye alichaguliwa kushika wadhifa huo tarehe 2, Novemba 1989. Kabla ya hapo, kwa muda wa miaka saba chama hicho kilikuwa kikiongozwa kwa mtindo wa Baraza la Uongozi. [5] Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah, Subhi Tufayli, Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah, Sheikh Naim Qassim, Hussein Kurani, Hussein Khalil, Muhammad Raad, Muhammad Fneish, Muhammad Yazbek na Ibrahim Amin ni miongoni mwa waliokuwa waasisi wa Hizbullah ya Lebanon. [6] Mei 1991 kutokana na kuzuka hitilafu na ukosoaji dhidi ya Subhi Tufayli, uongozi ulibadilishwa na Sayyid Abbas Musawi akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah. [7] Sayyid Abbas Musawi aliuawa shahidi na Israel Februari 16, 1992 na Baraza la Hizbullah likamchagua Sayyid Hassan Nasrullah kuwa Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah. [8]
Shakhsia Muhimu
Baadhi ya shakhsia muhimu wa Hizbullah ya Lebanon ni:
Sayyid Hassan Nasrullah
- Makala Asili: Sayyid Hassan Nasrullah
Sayyid Hassan Nasrullah (alizaliwa mwaka 1960) na ni Katibu Mkuu wa tatu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na kadhalika ni mmoja wa wajumbe waandamizi wa harakati hiyo. [9] Kipindi fulani Nasrullah alikuwa afisa mtendaji wa Hizbullah na amekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah tangu 1992. Katika kipindi cha uongozi wake, Israel iliondoka kwa madhila kusini mwa Lebanon mwaka 2000 na ikawaachilia huru mateka wa Kilebanon.
Sayyid Abbas Musawi
- Makala Asili: Sayyid Abbas Musawi
Sayyid Abbas Musawi (1952-1992) ni mjumbe muasisi na Katibu Mkuu wa pili wa Hizbullah. Alichukua jukumu na wadhifa wa ukatibu mkuu mwaka 1991 baada ya kuondolewa uongozini Subhi Tufayli. [10] Katika kipindi cha uhai wake alitumia muda wake mwingi akiwa pamoja na Wapalestina kuendesha mapambano dhidi ya Israel. Kipindi cha uongozi wake kama Katibu Mkuu wa Hizbullah kilikuwa chini ya miezi 9 na aliuawa shahidi na utawala wa Kizayuni wa Israel. [11]
Subhi Tufayli
- Makala Asili: Sheikh Subhi Tufayli
Sheikh Subhi Tufayli (alizaliwa 1948) ni Katibu Mkuu wa kwanza wa Hizbullah ya Lebanon na alishikilia wadhifa huo kuanzia 1989-1991. [12] Mnamo mwaka 1998, Tufayli aliasisi Thawrat al-Jiya (Mapinduzi ya Wenye Njaa). Wafuasi wake walivamia vituo vya serikali na kupelekea kuibuka mapigano yaliyosababisha idadi kati yao kuuawa. [13] Yeye ni katika wakosoaji wa Hizbullah ya Lebanon na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. [14]
Imad Mughniyah
- Makala Asili: Imad Mughniyah
Imad Mughniyah maarufu kama Haj Ridhwan alikuwa mmoja wa makamanda muhimu na mahiri wa Hizbullah. Alikuwa kamanda wa gadi ya ulinzi wa viongozi wa ngazi za juu na alikuwa na jukumu la operesheni maalumu za Hizbullah. Kadhalika alikuwa mpangaji na kiongozi wa operesheni za al-Waad al-Swadiq na kamanda katika medani ya Vita vya Siku 33 kati ya Hizbullah na Israel. [15] Israel ilimuua shahidi Imad Mughniyah Februari 12, 2008 katika mji mkuu wa Syria, Damascus. [16]
Kukabiliana na Israel
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon mwaka 1985 ilitangaza rasmi itikadi na stratejia yake ya kukabiliana na Israel. [17] Harakati za Hizbullah katika miaka ya awali ya kuasisiwa kwake zilijikita zaidi katika operesheni za kujitolea kufa shahidi dhidi ya wanajeshi wa Israel; lakini hatua kwa hatua mbinu hii ikabadilika. Wapiganaji wa Hizbullah katika kujibu kitendo cha kinyama cha kumuua shahidi Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Hizbullah wakati huo, kwa mara ya kwanza walivurumisha makombora ya katyusha kuelekea katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina. [18]
Baadhi ya matukio muhimu baina ya Hizbullah na Israel ni:
Operersheni ya al-Waad al-Swadiq
- Makala Asili: Vita vya siku 33
Katika mwaka 2006 kulitokea vita baina ya Hizbullah na Israel ambavyo vinatambulika kwa jina la Vita vya Tammuz au vita vya siku 33. Israel ilikiuka makubaliano yake na Hizbullah baada ya kuwaachia huru mateka wawili wa Kilebanon. Hizbullah ikiwa na lengo la kuwakomboa mateka hao, Julai 2006 ilianzisha operesheni ya kijeshi ya al-Waad al-Swadiq na kuwachukua mateka wanajeshi wawili wa Israel. Utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa na lengo la kuwakomboa wanajeshi wake hao na vilevile kama ulivyodai, kuipokonya silaha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon uliishambulia kijeshi Lebanon na hivyo kupelekea kuibuka vita baina ya Israel na Hizbullah ambavyo vilidumu kwa muda wa siku 33. [19]
Mapigano ya 1993
Julai 25, 1993 Israel iliishambulia Lebanon kwa minajili ya kuipokonya silaha Hizbullah, kuzusha mpasuko na mgawanyiko kuhusiana na Hizbullah na wananchi na wakati huo huo kuishinikiza serikali ya Lebanon ili izuie muqawama. Shambulio hilo lilikabiliwa na jibu kutoka kwa Hizbullah na pande mbili Julai 31, 1993 zilifikia makubaliano ya Julai. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Hizbullah ilikubali kusitisha uvurumishaji wa makombora ya Katyusha katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (zenye jina bandia la Israel) na mkabala wake Israel isitishe hujuma yake. [20]
Mapigano ya Aprili 1996
Aprili 11, 1996, Israel ilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Lebanon iliyojulikana kwa jina la Grapes of Wrath. Operesheni hii ni mashuhuri kwa kutekeleza mauaji manne ya umati ya Sahmar katika siku ya pili, shambulio dhidi ya gari la wagonjwa huko Mansouri katika siku ya tatu, Nabtiya Fawqa na Qana katika siku ya saba. Katika operesheni hii watu 24 wakiwemo wapiganaji 14 wa Hizbullah waliuawa shahidi. Operesheni hii ilidumu kwa muda wa siku 16 na hatimaye Israel na Hizbullah zikafikia makubaliano ya Aprili. Katika makubaliano haya, Israel iliahidi kutoshambulia raia na kwamba, katika mapigano yake itakabiliana tu na wapiganaji wa muqawama. [21]
Operesheni ya Ansariya
Hizbullah ilitekeleza operesheni ya Ansariya 5/9/1992 kwa ajili ya kukabiliana na hujuma na uvamizi wa makomando wa Israel. Operesheni hiyo ilipelekea kuuawa na kujeruhiwa Wazayuni 17. [22]
Kuwakomboa Mateka wa Muqawama
Baada ya jeshi la Israel kuondoka kusini mwa Lebanon, baadhi ya wanachama wa Hizbullah kama Mustafa Dirani na Sheikh Abdul-Karim Obeid walikuwa katika magereza ya Israel. Hizbullah ilitekeleza operesheni ya mashamba ya Shaba’a kusini mwa Lebanon na 7 Oktoba 2000 ikawakamata mateka wanajeshi watatu wa Israel. Aidha wanamapambano wa Hizbullah walimkamata kanali mmoja wa Kiisrael huko Beirut. Mkabala na kuwachia huru watu wake hawa, Israel ililazimika kuwaachilia huru Walebanon kadhaa na Wapalestina 400 sambamba na miili 59 ya mashahidi. Kadhalika ilifichua hatima ya watu 24 waliokuwa wamepotea sambamba na kutoa ramani ya mabomu ya kutegwa ardhi katika mipaka ya Lebanon. Shughuli ya ubadilishanaji ilifanyika tarehe 29 na 30 Januari 2004. [23]
Kufuatia vita vya siku 33, mwaka 2007 Hizbullah ilifanya mazungumzo na Israel kwa upatanishi wa Ujerumani na natija ya mazungumzo na upatanishi huo ikawa ni Israel kuwaachilia huru mateka wa Kilebanon waliokuwa wamebakia. Aidha miili ya mashahidi wa muqawama katika vita vya siku 33 na miili ya mashahidi wengine wa muqawama wa Lebanon na Palestina ukiwemo mwili wa Dalal al-Mughrabi na kundi lake la watu 12 nayo Israel iliikabidhi. [24]
Uwepo wa Hizbullah Syria kwa Ajili ya Kupambana na Daesh
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ilishirikiana na serikali ya Syria katika kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh. Baada ya kuibuka machafuko Syria, Hizbullah ilikuwa pamoja na jeshi la Israel katika vita dhidi ya matakfiri. [25] Kukombolewa mji wa al-Qusayr ulikuwa ni miongoni mwa ushindi muhimu wa Hizbullah huko Syria. [26]
Harakati za kisiasa
Hizbullah ilishiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Lebanon mwaka 1992 na kufanikiwa kupata viti 12 vya Bunge. Mwaka 1996 ilipata viti 10, na mwaka 2000 ikapata viti 12 kati ya 128 vya Bunge la Lebanon. [27] Katika uchaguzi mkuu wa 2005 katika kiwango cha nchi Hizbullah ilijinyakulia viti 14 vya Bunge peke yake. Kusini mwa Lebanon Hizbullah ilipata viti 23 baada ya kuunda muungano na Harakati ya Amal na ikamteua Muhammad Fneish kwa ajili kushika wadhifa wa Waziri wa Maji na Nishati. [28]
Baada ya mwaka 2005, Hizbullah ikawa katika makundi ya Machi 8. Mwaka 2005 sambamba na kuuawa Rafiq al-Harir aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon, kuliibuka muundo mpya katika uga wa siasa za nchi hiyo. Kundi la Machi 8 liliundwa kufuatia kongamano la Hizbullah mjini Beirut 2005 na kupinga kupokonywa silaha kundi hili, uungaji mkono wake kwa Syria na muqawama dhidi ya Israel; kambi ya muungano ambayo iliundwa kutokana na Hizbullah, Chama cha Amal, chama Free Christian ambapo baadaye mirengo mingine kama Jamaat al-slamiya, Harakati ya Tawhid (ya Waislamu wa Kisuni Lebanon Democratic Party (Druze) ilijiunga na kambi hii. [29]
Harakati ya Machi 14 iliibuka sambamba na himaya na uungaji mkono wa mataifa kama Marekani, Ufaransa, Saudi Arabia na Misri na kutaka Syria iondoke Lebanon na kupokonywa silaha muqawama. Harakati ya al-Mustaqbal (ya Kisuni), Hizb al-Kataib (The Kataeb Party) na Chama cha Maendeleo cha Kisoshalisti cha Wadruzi wa Lebanon (The Progressive Socialist Party) yalikuwa makundi makuu yaliyokuwa yakiunga mkono harakati hii.
Harakati za Kijamii
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imejikita zaidi katika suala la muqawama na kupambana na hujuma na uvamizi wa Israe; lakini pamoja na hayo, chama hiki kinafanya pia harakati mbalimbali za kijamii na miongoni mwazo ni:
- Kuanzisha taasisi za jihadi ya ujenzi kwa ajili ya kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na hujuma na mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel na majanga ya kimambile kama mafuriko, tetemeko la ardhi n.k
- Kukusanya takataka za mji katika vitongoji na viunga vya kusini mwa Beiruti kuanzia 1988-1991.
- Kutoa huduma ya maji kwa wakaazi wa maeneo ya kando kando kusini mwa Beirut.
- Harakati za kilimo.
- Kuanzisha Jumuiya ya Kiislamu ya afya na vituo vya matibabu pamoja na hospitali.
- Kutoa huduma za kielimu, mafunzo na misaada ya kimasomo kwa wanafunzi.
- Kuanzisha taasisi ya shahidi kwa ajili ya kutoa huduma kwa familia za mashahidi.
- Kuanzisha Taasisi ya Misaada ya Khei ya Kiislamu kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. [31]
Vyombo vya habari
- Kanali ya Televisheni ua al-Manar: Ilianzishwa 1991 (تلویزیون المنار).
- Idhaa ya al-Nour (https://www.alnour.com.lb). Idhaa hii iliasisiwa 1998.
- Jarida la wiki la al-Ahad (https://www.alahednews.com.lb) [32].
- Mtandao wa Intaneti wa Qawem https://qawem.org.
- Mtandao wa Intaneti kusini mwa Lebanon https://www.southlebanon.org
- Mtandao wa Intaneti wa mahusiano ya kihabari ya Hizbullah https://www.mediarelations-lb.org.
Hizbullah kadhalika imebadilisha moja ya kambi zake katika eneo la Melita kuwa makumbusho. [33]
Waungaji Mkono na Wapinzani wa Hizbullah
Hizbullah ina watu wanaoiunga mkono duniani. Mataifa muhimu yanayoiunga mkono Hizbullah ni Iran na Syria. Russia pia inaihesabu Hizbullah kama harakati halali ya kisiasa-kijamii [34]. Iran ilikuwa nafasi na mchango katika kuasisiwa Hizbullah na kutoa mafunzo kwa vikosi vyake. [35] Kadhalika Iran ilianzisha kamati ya ukarabati wa Lebanon lengo likiwa ni kukarabati maeneo yaliyobomolewa kufuatia hujuma na mashambulio ya Israel nchini Lebanon. [36] Pamoja na hayo, Marekani, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi nk. ziliitangaza Hizbullah au sehemu katika sehemu ya kijeshi ya harakati hiyo kuwa kundi la kigaidi. [37] Kukabiliana na uvamizi, vitisho vya Israel na kutokuwa na uwezo jeshi la Lebanon kukabiliana na Israel ni hoja zinazotolewa na watu wanaoamini kwamba, Hizbullah sio kundi la kigaidi na linapaswa kumiliki silaha. [38]
Bibliografia
Kumeandikwa vitabu mbalimbali uhusiana na Hizbullaha ya Lebanon. Miongoni mwa vitabu hivyo ni: Hizbullah al-Manhaj al-Tajribah al-Mustaqbal Lubnan wa muqawamatuh fil alwajihah, kimeandika na Sheikh Naim Qassim, mmoja wa viongozi wa Hizbullah ya Lebanon. Katika kitabu hiki, mwandishi anabainisha historia fupi, malengo na harakati za Hizbullah. [39] Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha ya Kifarsi kikiwa na anuani ya «Hizbullah Khatt Mish, Gozashteh va Mustaqbal An». [40]
Rejea
Vyanzo