Uga sumaku
Uga sumaku (ing. magnetic field) ni nafasi karibu na sumaku au mkondo wa umeme ambamo kani inaathiri magimba ndani yake. Uga sumaku hauonekani kwa macho lakini unapimika.
Kipimo cha SI kwa kutaja nguvu ya uga sumaku ni Tesla lakini mara nyingi kipimo cha kale cha Gauss kinatumiwa pia. Nguvu ya ugasumaku inapungua kadri ya umbali na chanzo chake.
Dunia ina ugasumaku unaosababishwa na kuzunguka kwa Dunia kunachofanya pia kiini kiowevu cha Dunia kuzunguka; ilhali kiini hiki kina chuma kingi kinafanya kazi kama dainamo. Ugasumako wa Dunia unasababisha sumaku kuelekea kaskazini penye ncha sumaku ya Dunia. Ugasumaku huu ni muhimu kwa uhai duniani kwa sababu unaelekeza sehemu kubwa ya mnururisho kutoka Jua kupita sayari yetu.
Nyota zote huwa pia na ugasumaku.