Nenda kwa yaliyomo

Lithi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Lithi
(Lithium)
Jina la Elementi Lithi
(Lithium)
Alama Li
Namba atomia 3
Mfululizo safu Metali alikali
Uzani atomia 6.941
Valensi 1
Densiti 0.534
Ugumu (Mohs) 0.6
Kiwango cha kuyeyuka 453.69 K (180.54 °C)
Kiwango cha kuchemka 1615 K (1342 °C)
Asilimia za ganda la dunia 0.006 %
Hali maada imara

Lithi ni elementi na metali alikali yenye namba atomia 3 na uzani atomia 6.941 kwenye mfumo radidia. Alama yake ni Li. Jina linatokana na Kigiriki λίθος líthos "mwamba, jiwe" kwa sababu iligunduliwa mara ya kwanza ndani ya miamba.

Lithi ni elementi nyepesi kabisa kati ya elementi zote zilizo imara kwa hali ya kawaida. Inamenyuka haraka na maji, hivyo husababisha majeraha ikiguswa kwa mkono kwa sababu mmenyuko wake na unyevu wa ngozi.

Kwa asili haipatikani kama dutu sahili kwa sababu inamenyuka haraka kikemia lakini iko kwa kampaundi mbalimbali, hasa katika miamba ya itale. Lithi tupu inapatikana kwa njia ya kikemia na inaonekana kama metali nyepesi yenye rangi nyeupe-kifedha lakini haibaki hivyo kwa muda mrefu. Katika hewa yenye unyevu uso wake huwa haraka ganda la hidroksidi ya lithi yenye rangi ya kijivu. Kwenye hewa kavu uso huwa nitriti ya lithi yenye rangi kahawia. Kwa sababu ya mimenyuko hiyo ya haraka lithi ya kimetali hutunzwa ndani ya mafuta.

Lithi

Matumizi yake ni ndani ya betri na katika dawa mbalimbali. Betri za kisasa zinazotumiwa katika simu za mkononi karibu zote zinatumia lithi. Mipango ya kutengeneza magari ya umeme inategemea betri za lithi na hivyo imetabiriwa ya kwamba bei yake itapanda.

Kuna isotopi 5 za lithi zenye neutroni 2, 3, 4, 5 na 6 kwenye kiini atomia. Isotopi ya kawaida ni 3Li7 ambayo ni 92.58 % ya lithi yote duniani. Nyingine ni 3Li6 yenye 7.42 % ya lithi yote. Nyingine zinapatikana kidogokidogo tu.

Makala hii kuhusu mambo ya kemia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Lithi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.